Bingwa wa Olimpiki wa mbio za
walemavu Oscar Pistorius, ataachiliwa huru kutoka gerezani Jumanne na
kuwekwa kwenye kizuizi cha nyumbani.
Huo ndio uamuzi uliofikiwa na bodi ya kutoa msamaha kwa wafungwa nchini Afrika Kusini.Pistorius alifungwa jela miaka mitano mwaka 2014 baada ya kupatikana na makosa ya kuua bila kukusudia.
Alifungwa jela kwa kumuua mpenzi wake Reeva Steenkamp kwa kumpiga risasi akiwa kwenye bafu.
Akijitetea, Pistorius alisema alimpiga risasi akidhani ni mtu kutoka nje aliyekuwa ameingia nyumbani kwake.
Upande wa mashtaka umekata rufaa ukisema alifaa kuhukumiwa kwa mauaji.
Rufaa hiyo itasikizwa Novemba 3.
Pistorius amekaa jela miezi 12 na sasa atatumikia kipindi kilichosalia cha kifungo chake chini ya “uangalizi wa maafisa wa magereza,” bodi hiyo ya msamaha imesema.
Uamuzi wa awali wa kumwachilia huru Agosti ulisimamishwa na Waziri wa Haki wa Afrika Kusini Michael Masutha, aliyesema uamuzi huo ulikuwa umefanywa “mapema mno”.
Wakati huo, familia ya Bi Steenkamp ilisema miezi 10 ilikuwa “haitoshi”.
Akizungumzia uamuzi wa sasa hivi, wakili anayewakilisha familia ya Steenkamp alisema wazazi wake walitarajiwa aachiliwe mapema, ingawa hawakuwa wanauunga mkono uamuzi huo.
Aliongeza kuwa hakuna lolote linaloweza kumfufua binti yao.
Familia ya Pistorius imesema imepokea habari za kuachiliwa huru kwake, lakini ikakataa kuzungumzia suala hilo zaidi.
No comments:
Post a Comment