MWANAMKE mkazi wa kijiji
cha Ikandamoyo, wilayani
Katavi, Veronica Saleh ‘Mama
Kaela’ (50), amefanya uamuzi
adimu wa kuolewa na
wanaume wawili ambao
anaishi nao kijijini hapo.
Kijiji hicho kipo umbali wa
takribani kilometa 30 kutoka
mjini hapa katika Jimbo la
Katavi linalowakilishwa na
Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Pamoja na ndoa hiyo
iliyowezeshwa na mume
mkubwa kukubali kuishi na
mume mdogo, imeelezwa kuwa
mwanamke huyo ndiye
‘aliyewaoa’ wanaume hao kwa
zaidi ya miaka saba sasa, huku
akiwa na amri kuu katika
nyumba, kama ilivyo katika
ndoa za kawaida.
Wanaume hao ni Paulo Sabuni
‘Baba Kaela’ (60) ambaye
ndiye mume mkubwa na
Arcado Mlele (45) ambaye ni
mume mdogo.
Taarifa za kuwapo kwa ndoa
hiyo ya aina yake, ziliifikia
BLOG HII na kufanyiwa
uchunguzi kwa zaidi ya wiki
tatu, na hatimaye katikati ya
wiki hii, wahusika walikubali
wao wenyewe kuzungumzia
suala hilo. Kwa mujibu wa
maelezo ya mwanamke huyo
ambaye alionekana kuwa
msemaji wa familia hiyo, yeye
na mumewe mkubwa, walifika
kijijini hapo miaka 24 iliyopita,
wakitoka kijiji cha Usumbwa
mpakani mwa Chunya, Mbeya
na Tabora.
Wakiwa kijijini hapo mume
wake aliendelea kufanya kazi
ya ukulima wakati yeye mama
(Veronica), pamoja na kilimo
hujihusisha na upishi na uuzaji
wa pombe ya kienyeji iitwayo
kayoga.
Mwanamke huyo ambaye
amesema ana watoto wanne,
Alfred (20), binti mwenye
miaka 16 (ambaye ameolewa)
na wengine wawili wa kiume,
mmoja akisoma darasa la sita
na mdogo ana miaka saba,
amesema hana shida na
waume wake.
Ingawa wanandoa hao
walizungumza kwa hadhari,
majirani walikiri kuwa
mwanamke huyo anaishi na
wanaume hao wawili kwa
amani na kwamba mwanamke
huyo ndiye mwenye sauti na si
waume zake.
“Si siri tena sasa,
tumeshawazoea, kwani
wanaishi kwa amani ila yule
mume mdogo anaishi kwenye
nyumba aliyoachiwa na
marehemu baba yake, lakini
anashinda kwa mume
mkubwa, ambapo inajulikana
kijijini hapa kuwa ni nyumba
kubwa. “Basi pale ni mambo
yote, kula na kunywa, mama
huyu amewapangia zamu
wanaume hao kama afanyavyo
mume mwenye wake wengi.
Ama kweli ukistaajabu ya
Musa utaona ya Firauni,”
alisema mkazi mmoja kwa
masharti ya jina lake
Kutotajwa
Alielezwa, kwamba wanaume
hao wana akili timamu na
hawatumii kilevi cha pombe
kama ilivyo kwa mke wao.
Hata hivyo, mume mkubwa
anapewa sifa za upole tofauti
na mume mdogo anayetajwa
kuwa mkorofi kiasi cha mara
kadhaa kumchapa makofi
mkewe anapomuudhi.
Majirani wanadai kwamba
Mama Kaela na mumewe
Paulo, walipofika kijijini hapo,
walipokewa na kuishi maisha
ya kawaida, lakini baadaye
mama huyo alianza kuwa na
uhusiano wa kimapenzi na
Arcado, ambaye naye
alilazimika kuachana na
mkewe wa ndoa
anayefahamika kijijini hapo
kwa jina la Mama Pere.
Ilielezwa na mashuhuda hao
kwamba mume mkubwa
alipobaini uhusiano huo,
alikuja juu, lakini mwanamke
huyo inadaiwa alimweleza
mumewe huyo, atake asitake
lazima wataishi wawili,
vinginevyo ataachana naye,
ndipo mume mkubwa
alipokubali kuishi na mume
mwenza.
Katika maisha ya kawaida
katika familia hiyo, inaelezwa
kwamba katika baadhi ya siku
ikitokea kuwa mama huyo
amechoka kupika, mume
mdogo huchukua jukumu la
kupika na kumwandalia
chakula na maji ya kuoga
mume mkubwa.
“Lakini mara nyingi kwa
mfano, ikiwa ni zamu ya
mama huyo kulala kwa
mumewe mkubwa, basi
humfulia nguo zake kisha
anakwenda kwa mumewe
mdogo nako anamfulia nguo.
“Ndivyo wanavyoishi, nasi
sasa tumewazoea ila yule
mama ni mkali na ana sauti
pale kwake kwa wanaume
wale ila tunaona kama ana
wivu sana kwa huyu mdogo
ambaye naye pia ana wivu
kwa mkewe huyo, labda
anahofia kuwa mama huyo
anaweza kuongeza
mwanamume mwingine,”
anasema mmoja wa majirani
hao.
Hakuna mazuri yasiyokuwa na
machungu, japo familia hiyo
inaelezwa kuwa na amani,
mtoto wao mdogo nusura
avuruge uhusiano wa
wanandoa hao, baada ya
kuibuka mzozo wakati wa
maandalizi ya ubatizo wake.
Kwa sababu anazojua mama,
ingawa inafahamika kuwa
wote ni watoto wa mume
mkubwa, mke huyo katika hati
za ubatizo aliandikisha ubini
wa mtoto huyo kuwa ni Mlele
(akimaanisha kuwa mtoto wa
mume mdogo), lakini mume
mkubwa aliweka pingamizi
kanisani akidai yeye ndiye
baba halali wa mtoto huyo.
Kwa mujibu wa mwanamke
huyo, yeye na Arcado ni
waumini wa madhehebu ya
Katoliki wakati Paulo ni
Mpentekoste. Madai ya mzozo
wa uhalali wa `ubaba’ wa
mtoto huyo, yalithibitishwa na
baadhi ya wakazi wa kijiji
hicho, akiwamo mwalimu wa
dini wa Kigango cha Kanisa
Katoliki Uruira, Mashaka Abel.
Walisema miaka sita iliyopita,
mtoto huyo akiwa na umri wa
mwaka mmoja, alifanyiwa
taratibu za ubatizo, lakini
ilishindikana, kutokana na
wanaume hao, kila mmoja
kudai ndiye baba mzazi wa
mtoto.
“Lilikuwa jambo la
kustaajabisha sana, kwani
familia hiyo ilifanya
maandalizi yote ya sherehe ya
ubatizo wa mtoto huyo, lakini
siku hiyo kanisani wakati huo
ilikuwa ni kigango cha
Katumba ambacho sasa ni
Uruira, sakata lilianzia pale
Padri alipomwuliza mama wa
mtoto huyo ubini wa mtoto
naye akasema ni Mlele.
“Hapo ndipo mume mkubwa
alipopinga na kudai kuwa
mtoto yule si wa Arcado bali
wake na yeye ndiye baba
halali. Padri hakuamini,
aliuliza tena na tena na majibu
yakawa ni yale yale, ndipo
ubatizo ukashindikana,”
alisema Katekista Abel.
Kazi ya kutafuta undani wa
ndoa hiyo haikuwa rahisi
kutokana na mazingira ya
woga na usiri uliokusudiwa
kubaki, ambapo awali mama
alisema kwamba mume wake
ni Paulo pekee japo siku
ambayo mwandishi wa habari
hizi alifika kijijini hapo na
baadaye nyumbani kwa
wanandoa hao na kumkuta
mume mdogo (Arcado
akimsaidia mkewe kukoroga
pombe. Awali katika
utambulisho, walidai kuwa ni
mtu na mdogo wake na kusita
kuzungumzia maisha yao ya
kifamilia.
Mke wao ambaye alionekana
wazi kuwa ni msemaji mkuu
alifoka na kuja juu, akidai
kuwa hayuko tayari
kuzungumzia uhusiano wake
na wanaume hao wawili,
ingawa alikiri kuwa wanaishi
pamoja.
"Kwa hiyo umefunga safari
yote hii kutoka huko ulikotoka
ili uje kwangu mie Veronica …
nasema sitaki kabisa mtu kuja
hapa na kutaka kunivurugia
mpangilio wa maisha yangu,
kwanza nani alikueleza hayo,
wambea wakubwa hao
yanawahusu nini watu hao?”
alihoji.
“Mie mume wangu ni huyu
Paulo basi … sasa leo
umeniachia vurugu ndani ya
nyumba nitapigwa na huyo
mume wangu Paulo, kwani
mmenishikisha ugoni?” alifoka
Mama Kaela. Hata hivyo,
mume mkubwa alidai kuwa
hatamwadhibu mkewe huyo na
kwamba wataendelea kuishi
pamoja na mdogo wake
Arcado kwa amani. Hata
hivyo, akina mama wengi
kijijini hapo wanalaani kitendo
cha mama huyo kuishi na
wanaume wawili ambapo
waliomba uongozi wa Kanisa
uingilie kati, ili mama huyo
aweze kufunga ndoa na mume
mmoja.
Lakini kwa upande mwingine,
baadhi walimpongeza
mwanamke huyo wakidai
kuwa kitendo hicho ni cha
kijasiri kwa mwanamke,
kumudu kuishi na wanaume
wawili na kuwa na mamlaka
juu yao.
ABC
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment