Uchunguzi wa kisasa uliofanyiwa
kaburi la mwandishi mashuhuri William Shakespeare umeonesha huenda fuvu
la kichwa chake liliibiwa.
Ugunduzi huo unaonekana kutoa uzito kwa
ripoti zilizochapishwa katika vyombo vya habari 1879, ambazo baadaye
zilipuuziliwa mbali na kutajwa kuwa uvumi, kwamba kuna watu walioiba
fuvu hilo mwaka 1794.Kundi la watafiti lilitumia teknolojia inayoweza kupenya ardhini (GPR) kutazama ndani ya kaburi hilo katika kanisa la Holy Trinity, Stratford ambao ni uchunguzi wa kwanza wa kiakiolojia kufanyiwa kaburi hilo.
Teknolojia hiyo iliwawezesha kuangalia ndani ya kaburi hilo bila kulifungua.
Mwanakiolojia Kevin Colls kutoka chuo kikuu cha Staffordshire, aliyeongoza uchunguzi huo akishirikiana na mtaalamu mwingine Erica Utsi, amesema: "Tumeangalia alimozikwa Shakespeare na tukaona kuna kasoro pahala ambapo kichwa chake kinafaa kuwa na kuna taarifa zinazodokeza kwamba huenda wakati mmoja kuna mtu aliiba fuvu la kichwa cha Shakespeare.
"Hili linanishawishi sana kuamini kwamba fuvu lake haliko katika kanisa la Holy Trinity kamwe."
Uchunguzi huo ulikuwa sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya miaka 400 tangu kifo cha Shakespeare.
Kaburi ambamo Shakespeare alizikwa mwaka 1616 limeandikwa onyo na kulaani mtu ambaye atathubutu kufungua kaburi lake.
No comments:
Post a Comment