Breaking News
recent

Unakumbuka Stori ya Uingereza kupoteza kombe la dunia mwaka 1966?

Mwaka 1966 fainali za Kombe la Dunia ziliandaliwa nchini Uingereza na wenyeji wakashinda lakini nusura kukosekane kombe la kuwazawadi baada ya kombe hilo kuibiwa.
Uingereza walitwaa ushindi kwenye fainali ya kihistoria dhidi ya Ujerumani.
Kombe lilikuwa limewekwa kwa maonesho katikati mwa London kabla ya michuano kuanza lilipoibiwa licha ya kuwa chini ya ulinzi mkali wa polisi saa 24.
Taarifa baadaye lilisema afisa aliyekuwa analilinda wakati huo alikuwa ametoka kwenda kutafuta chakula lilipotoweka.
Polisi walishindwa kupiga hatua katika uchunguzi wao, sawa na wachunguzi wasifika wa jinai wa Scotland Yard.
Matumaini ya kulipata kombe hilo la Jules Rimet yalikuwa yamefifia wiki moja yaa kuibiwa.
Mbwa kwa jina Pickles ndiye aliyeokoa hali.
Alikuwa ametolewa nje kwa matembezi na mmiliki wake Dave Corbett kama ilivyokuwa kawaida kila siku.
“Watu walikuwa wanaamini kwamba polisi hawangeweza kukipata kikombe hicho,” anasema Bw Corbett, ambaye alikuwa shabiki sugu wa soka.
“Nilimtoa mbwa wangu kwa matembezi na akakimbia na kufika mbele ya gari la jirani na akaanza kunusanusa. Nilifika hapo ili kumfunga mnyororo, na nikagundua kulikuwa na kitu chini, kimefungwa kwa magazeti na kamba juu yake. Nilikichukua kitu hicho. Nilirarua karatasi kidogo na nikaona jina Brazil, Ujerumani Magharibi...”
Alikuwa tayari anafahamu habari za kupotea kwa kikombe hicho na alijua bila shaka kilikuwa kikombe kilichokuwa kikitafutwa na polisi.
Alikimbia mara moja hadi kituo cha polisi kilichokuwa karibu. Hata hakukumbuka kubadilisha mavazi.
Alimkuta afisa aliyekuwa zamu na kumwambia: "Nadhani nimelipata Kombe la Dunia”.
Afisa huyo alimwita mkubwa wake ambaye mara moja aliagiza Corbett apelekwe kwa Scotland Yard.
Ni hapo ambapo aligundua kwamba alikuwa sasa: "Mshukiwa nambari moja”.
Lakini baada ya kuhojiwa ikabainika kwamba hakuhusika katika wizi na sasa akawa shahidi. Washukiwa halisi walikamatwa na kushtakiwa.
Mbwa wake kuanzia hapo aligeuka na kuwa shujaa wa taifa.
Walialikwa, Corbett na Pickles, kwa hafla ya kusherehekea ushindi wa Uingereza jijini London.
Bobby Moore, aliyekuwa nahodha wa timu ya taifa ya Uingereza, alimuinua Pickles na kumuonesha kwa watu waliohudhuria sherehe hiyo.
Pickles pia alizawadiwa nishani na mfupa wa bata, na wawili hao kwa pamoja wakapewa hundi ya pauni 1,000.
Kwa kutumia pesa hizo, Corbett, alinunua nyumba. Mbwa huyo alifariki 1967.
Pickles alibadilisha maisha ya Corbett na hadi sasa hajamsahau mbwa huyo ambaye kwa utani humuita Picks.
Huwa anatembelea kaburi lake mara kwa mara. Kaburi ya Pickles limeandikwa "Pickles: Aliyelipata Kombe la Dunia”.

ABC

ABC

No comments:

Post a Comment

Powered by Blogger.